Nenda kwa yaliyomo

Mfumo wa mzunguko wa damu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Circulatory system)
Moyo na mishipa ya damu
Ateri ndogo ("aterioli") na vena ndogo ("venuli") zinakutana kwenye kapilari

Mfumo wa mzunguko wa damu (ing. circulatory system) ni jumla ya mishipa ya damu mwilini pamoja na moyo. Ni sehemu muhimu ya uhai wa viumbe wengi (lakini si wanyama wote).

Kazi ya mzunguko wa damu

Mzunguko wa damu unafikisha mwilini mwote virutubishi, oksijeni, homoni na seli za damu ili kulisha, kukinga dhidi ya maradhi, pamoja na kudhibiti halijoto na uwiano kwa jumla.

Damu ni chombo cha kusafirisha mahitaji ya seli kama vile virutubishi na oksijeni pale panapohitajika, halafu inapokea dutu zisizohitajika tena kutoka seli na kuzipeleka kwa viungo zinapoondolewa mwilini.

Ateri, vena, kapilari

Moyo ni ogani inayosukuma damu katika mishipa yake ambayo husafirisha damu kwenda sehemu zote za mwili ili ziweze kutenda kazi.

  • Ateri ni mishipa inayopeleka damu kutoka moyoni kwenda mwilini.
  • Vena ni mishipa inayopeleka damu kuingia moyoni kutoka mwilini.

Ateri huwa nyembamba zaidi kadri zisivyofika mbali na moyo. Mwishoni ni nyembamba sana huitwa aterioli na kuingia katika kapilari ambazo ni vyombo vya damu vyembamba mno zinazolisha seli za mwili moja kwa moja.

Vivyo hivyo vena zinaanza kwa umbo neymbamba upande wa kinyume cha kapilari zikiitwa venuli. Zinaongezeka unene kadri zinavyokuwa karibu zaidi na moyo.

Kwa hiyo mwendo au mzunguko wa damu ni moyo - ateri - aterioli - kapilari - venuli - vena - moyo.

Mizunguko miwili

Mfumo wa mizunguko miwili ya damu

Kwa mamalia pamoja na binadamu mfumo wa mzunguko wa damu kwa jumla huwa na pande mbili:

  • mzunguko wa damu wa mwili wote ("systemic circulation")
  • mzunguko wa damu wa mapafu ("pulmonary circulation") unaopitisha damu kwenye mapafu wa kusudi la kuondoa hewa chafu na kuingiza oksijeni.

Pande hizi mbili za mzunguko zinashughulikiwa na pande mbili za moyo:

  • damu iliyoishia oksijeni inarudi moyoni kupitia vena. Inaingia nusu ya kulia ya moyo na kutoka hapa inasukumwa kwenda mapafu. Ndani ya mapafu gesi ya CO2 inaondolewa katika damu na oksijeni kuongezeka.
  • damu inarudi na kuingia katika moyo upande wa kushoto. Kutoka hapa damu yenye oksijeni inasukumwa katika ateri za kuipeleka kote mwilini.

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mfumo wa mzunguko wa damu kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.