Nenda kwa yaliyomo

Timur

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Timur alivyokuwa.
Milki ya Timur

Timur (8 Aprili 1336 - 19 Februari 1405) alikuwa kiongozi Mwislamu wa Waturuki na Wamongolia wa Asia ya Kati wakati wa karne ya 14 aliyeanzisha milki ya Watimuri.

Jina lake kamili Lilikuwa Timur bin Taraghay Barlas kutokana na neno la Kichagatai تیمور "chuma". Alijulikana pia kama Timur-e Lang yaani "Timur mlemavu" au Tamerlan. Aliitwa pia "Timur Mkuu".

Alizaliwa mjini Kesh (leo: Sachrisabz) karibu na Samarkand katika Uzbekistan wa leo.

Akianza kama chifu wa kabila dogo alipanda ngazi katika utumishi wa watawala wa Chagatai na kuchukua nafasi yao.

Baada ya kuoa binti wa ukoo wa Jingis Khan alilenga kurudia milki ya Jingis Khan kwa umbo la Kiislamu. Timur mwenyewe alikuwa Mwislamu mkali aliyelazimisha Wamongolia wote wa eneo lake kukubali Uislamu. Alipenda pia mila na desturi za Wamongolia wa kale kabla ya kugeukia Uislamu.

Kwa njia ya vita vingi alipanua milki yake. Alihofiwa kama kiongozi mkali bila huruma kwa maadui na wapinzani. Vita zake zakumbukwa kwa sababu ya idadi kubwa ya watu waliochinjwa na wanajeshi wake.

Kuna mifano mingi ya unyama wake. Baada ya jeshi lake kutwaa mji wa Isfahan (Uajemi) minara 28 ya vichwa vilihesabiwa, jumla ya watu 70,000 walichinjwa. Baada ya kutwaa Baghdad (1401) aliamuru maandamano ya wanajeshi mbele yake akadai kila askari ashike vichwa viwili vilivyokatwa.

Alichukia hasa Wakristo katika milki yake kwa sababu sehemu ya Wamongolia na Waturuki walifuata Ukristo wa Kinestorio. Chini ya Timur Ukristo wa Asia ya Kati ulipungua mno na kupotea kabisa katika nchi kadhaa.

Lakini alichukia pia Wahindu, akichinja wafungwa 100,000 wakati wa kushambulia Delhi mwaka 1398.

Aliaga dunia mjini Otrar katika Kazakhstan ya leo.

Baada ya kifo chake milki iliporomoka haraka kwa sababu ilijengwa kwa hofu bila utaratibu wa kiutawala.

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Timur kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.