Msamiati wa Teknolojia
Dijitali
A Lexicon of Key Words
     in Kiswahili
     Contributors:
       Rocha Chimerah
       Mwanahija Juma
       Consolata Mushi
      Kithaka wa Mberia
        Alfred Mtwali
        Kimani Njogu
        Salome Nduku
      Rayya Timmamy
    Rachael Ndichu-Ngugi
      Duncan Ogweno
Coordinated by Nanjala Nyabola
  Assisted by Eunice Njomo
 Designed by Kedolwa Waziri
          Made possible with support from the Stanford
                  Digital Civil Society Fellowship, 2021
1. Alogaridhimu (n)
  a. Utaratibu wa kufumbua mafumbo ya hisabati
  (kama vile kupata kigawo kikubwa cha nambari
  zote) kwa hatua zilizobainishwa, ambao mara
  nyingi hujumuisha kurudia ukokotoaji fulani;
  utaratibu wa hatua baada ya hatua wa
  kusuluhisha tatizo au kutimiza lengo fulani.
  Kanuni zinazotumiwa na kompyuta kuchambua
  fumbo la hisabati.
     Algorithm
       a. A procedure for solving a mathematical
       problem (as of finding the greatest common
       divisor) in a finite number of steps that frequently
       involves repetition of an operation broadly: a step-
       by-step procedure for solving a problem or
       accomplishing some end. The rules used by a
       computer to sort through a mathematical
       problem.
2. Upendeleo wa Alogaridhimu (n)
  a. Hurejelea makosa ya utaratibu na yanayoweza
  kurudiwa katika mfumo wa kompyuta ambayo
  huzalisha matokeo yasiyo na usawa, kama vile
  kunufaisha kikundi kimoja cha watumiaji zaidi ya
  kingine. Upendeleo unaweza kujitokeza kwa sababu
  nyingi, kama vile muundo wa alogaridhimu au
  matumizi yasiyonuiwa au yasiyotarajiwa au maamuzi
  yanayohusiana na jinsi data ilivyoainishwa, kukusanywa,
  kuchaguliwa au kutumiwa kufundisha alogaridhimu.
  Mifano ya upendeleo wa alogaridhimu ni pamoja na
  kutafsiri maneno yanayotaja jinsia kama ya kiume kama
  chaguo msingi, au kupatia matamshi ya chuki
  kipaumbele cha juu kuliko habari kwenye mitandao ya
  kijamii.
    Algorithmic Bias
       b. Describes systematic and repeatable errors in a
       computer system that create unfair outcomes,
       such as privileging one arbitrary group of users
       over others. Bias can emerge due to many factors,
       including but not limited to the design of the
       algorithm or the unintended or unanticipated use
       or decisions relating to the way data is coded,
       collected, selected or used to train the algorithm.
       Examples of algorithmic bias include translating
       gender neutral pronouns as masculine by default,
       or promoting hate speech over news in social
       media networks.
3. Uchanganuzi
  a. Mchakato wa kuchambua data ya msingi ili kupata
  maana yake. Uchambuzi makini na kamili wa data kwa
  kutumia kielelezo, kwa kawaida hufanywa na
  kompyuta; habari inayotokana na uchambuzi huu.
    Analytics
       b. The process of analysing raw data in order to
       make sense of that information. A careful
       and complete analysis of data using a model,
       usually performed by a computer; information
       resulting from this analysis.
4. Ufiche
  a. Hali ya kubaki bila kukujulikana na watu wengine
  walio wengi. Ufiche mtandaoni ni hali ya kuficha data
  yako ya kibinafsi, kama vile mahali ulipo, anwani yako
  ya IP, n.k. ili isionekane na tovuti unazotumia au
  watumiaji wengine.
    Anonymity
       b. The state of remaining unknown to most other
       people. Online anonymity refers to hiding your
       personal data like your location, IP address, etc.
       from the websites you use or from other users.
5. Akili unde/ Utafiti wa Akili Unde (n)
  a. Utafiti na ukuzaji wa mifumo ya kompyuta
  ambayo inaweza kuiga tabia za binadamu
  mwenye umaizi.
     Artificial intelligence
       b. The study and development of computer
       systems that can copy intelligent human
       behaviour.
6. Mtambowavu/ mitambowavu (n)
  a. Programu ya kompyuta inayotekeleza kazi za
  kiotomatiki kwenye wavuti, kama vile kudumisha
  uwepo kwenye mitandao ya kijamii.
     Bot/bots
       b. A computer program that runs automated
       tasks over the internet like maintaining a
       presence on social media.
7. Uwandaraia (n)
  a. Uwandaraia ni mazingira ya kisiasa, ya utungaji sheria,
  ya kijamii na ya kiuchumi yanayowawezesha raia
  kujumuika, kushiriki masilahi yao na masuala
  yanayowatatiza na kutenda kibinafsi na kwa pamoja
  kushawishi na kuelekeza uundaji wa sera. Uwandaraia
  huhimiza watu kuzingatia mitazamo mbalimbali,
  ambayo wakati mwingine hukinzana.
     Civic space
       b. Civic space is the political, legislative, social and
       economic environment which enables citizens to
       come together, share their interests and concerns
       and act individually and collectively to influence
       and shape the policy-making. Civic space
       encourages people to pursue multiple, at times
       competing, points of view.
8. Idhini ya Creative Commons (n)
  a. Leseni mbalimbali zinazowawezesha watu
  kushiriki kazi zao za hakimiliki ili ziweze
  kunakiliwa, kuhaririwa, kuendelezwa, n.k., huku
  wakibaki na hakimiliki ya kazi ya asili (mara nyingi
  hutumiwa kwa kumtambua mwenye hakimiliki).
     Creative Commons
        b. A set of various licenses that allow people to
        share their copyrighted work to be copied,
        edited, built upon, etc., while retaining the
        copyright to the original work (often used
        attributively).
9. Ukatili mtandaoni (n)
  a. Shughuli ya kutumia ujumbe kwenye mitandao ya
  kijamii, barua pepe, ujumbe mfupi, n.k. kumtisha au
  kumfadhaisha mtu.
     Cyberbullying
        b. The activity of using messages on social media,
        emails, text messages, etc. to frighten or upset
        somebody.
10. Ulinzi mtandaoni (n)
  a. Ulinzi mtandaoni ni shughuli za kulinda mitandao,
  vifaa na data dhidi ya ufikiaji usioruhusiwa au dhidi ya
  matumizi yaliyo kinyume cha sheria. Vilevile ni mbinu
  za kuhakikisha usiri, ukamilifu na upatikanaji wa habari.
     Cyber security
        b. Cybersecurity is the act of protecting networks,
        devices, and data from unauthorized
        access or criminal use and the practice of
        ensuring confidentiality, integrity, and
        availability of information.
11. Usalama mtandaoni (n)
  a. Hatua za kujaribu kuwa salama mtandaoni na
  vitendo vya kuongeza ufahamu wa mtumiaji
  kuhusu hatari zilizopo kwa usalama wake binafsi
  na kwa habari za kibinafsi na miliki inayohusiana
  na matumizi ya intaneti, pamoja na juhudi za
  kujilinda dhidi ya uhalifu wa kompyuta.
     Digital/ Internet safety
       b. The Act of trying to be safe on the internet and
       is the act of maximizing a user's awareness of
       personal safety and security risks to private
       information and property associated with using
       the internet, and self-protection from computer
       crime.
12. Data (n)
  a. Ukweli au habari, haswa inapochunguzwa na
  kutumiwa kubainisha mambo au kufanya maamuzi.
     Data
       b. Facts or information, especially when examined
       and used to find out things or to make decisions.
13. Faragha data (n)
  a. Faragha data au faragha ya habari ni tawi la ulinzi wa
  data linalohusika na utunzaji mzuri wa data - idhini,
  ilani na masharti ya kisheria. Hususan, masuala ya
  faragha data mara nyingi yanahusu ikiwa data
  inashirikiwa au jinsi inavyoshirikiwa na wengine.
     Data privacy
       b. Data privacy or information privacy is a branch
       of data security concerned with the proper
       handling of data – consent, notice, and regulatory
       obligations. More specifically, practical data
       privacy concerns often revolve around whether or
       how data is shared with third parties.
14. Ulinzi data (n)
  a. Udhibiti wa kisheria unaolinda faragha ya
  habari iliyohifadhiwa kwenye kompyuta na
  kuweka mipaka ya wanaoweza kuisoma au
  kuitumia.
     Data Protection
       b. Legal controls that keep information stored on
       computers private and that limit who can read it
       or use it.
15. Kuchunga data (n)
  a. Mchakato ambao kwa kawaida hufanyika kiotomatiki
  ambapo teknolojia huchukua data kutoka programu au
  tovuti fulani kwa matumizi mabalimbali; matokeo ya
  mchakato huu kwa kwa kawaida huwa mkusanyiko wa
  data inayoweza kuchambuliwa.
     Data Scraping
       b. A usually automated process where a
       technology takes data from a particular program
       or websites for a variety of uses that usually results
       in aggregation for analysis.
16. Limbiko data (n)
  a. Limbiko data ni mkusanyiko wa data ilyopangwa kwa
  utaratibu na ambayo kwa ujumla inahusishwa na kazi
  ya kipekee.
     Data Set
       b. A dataset is a structured collection of data
       generally associated with a unique body of work.
17. Hifadhidata (n)
  a. Hifadhidata ni mkusanyiko wa data iliyohifadhiwa
  kama limbiko data nyingi. Limbiko data hizo kwa
  ujumla huhifadhiwa na kupatikana kielektroniki
  kwenye mfumo wa kompyuta unaoruhusu data
  kufikiwa, kubadilishwa na kusasishwa kwa urahisi.
     Dataset
       b. A database is an organized collection of data
       stored as multiple datasets. Those datasets are
       generally stored and accessed electronically from
       a computer system that allows the data to be
       easily accessed, manipulated, and updated.
18. Ughushi mbizi (n)
  a. Media ya kubuniwa ambapo taswira ya mtu aliye
  katika picha au video ya asili hubadilishwa na kuwekwa
  taswira ya mtu mwingine, iliyoundwa kwa ufunzaji wa
  kina wa kompyuta na Akili Unde.
     Deepfakes
       b. Synthetic media in which a person in an
       existing image or video is replaced with someone
       else's likeness, created by deep learning and AI.
19. Utambulisho dijitali (n)
  a. Ni jumla ya habari mtandaoni kuhusu mtu binafsi,
  shirika au kifaa cha kielektroniki.
     Digital identity
       b. Is the body of information about an individual,
       organization or electronic device that exists
       online.
20. Umaizi dijitali (n)
  a. Umaizi dijitali ni uwezo wa kutumia teknolojia ya
  habari na mawasiliano kupata, kutathmini, kuzalishaa
  na kutoa habari; huhitaji ujuzi wa utambuzi na wa
  kifundi.
     Digital literacy
       b. Digital literacy is the ability to use information
       and communication technologies to find,
       evaluate, create, and communicate information,
       requiring both cognitive and technical skills.
21. Taarifa Potoshi (n)
  a. Habari ya uongo inayotolewa kwa makusudi.
     Disinformation
       b. False information that is given deliberately.
22. Ufichuzi Harabu (n)
  a. Kitendo cha kufichua hadharani habari za kibinafsi
  zilizokuwa za faragha hapo awali kuhusu mtu au
  shirika; kwa kawaida hufanyika mtandaoni.
     Doxing
       b. The act of publicly revealing previously private
       personal information about an individual or
       organization, usually through the Internet.
23. Ufichamishaji Kamili (n)
  a. Ulinzi wa data inayotumwa kupitia majukwaa dijitali
  ili iweze kusomwa na mtumaji na mpokeaji tu, hususan
  kuzuia mmiliki wa jukwaa asisome habari hizo na pia
  wengine wasiweze kuziingilia na kuzisoma.
     End-to-End Encryption
       b. The protection of data sent over digital
       platforms so that only the sender and the receiver
       can read it, particularly excluding the owner of the
       platform but also third party interference from
       reading the information.
24. Uhuru wa Kutangamana (n)
  a. Haki ya kukutana na watu na kuunda mashirika bila
  kuhitaji idhini kutoka kwa serikali.
     Freedom of Association
       b. The right to meet people and to form
       organizations without needing permission from
       the government.
25. Uhuru wa Kunena (n)
  a. Nguvu au haki ya mtu kutoa maoni bila udhibiti,
  kizuizi au adhabu ya kisheria.
     Freedom of Expression
       b. The power or right to express one's opinions
       without censorship, restraint, or legal penalty.
26. Uhuru wa maoni (n)
  a. Haki ya kutoa maoni yoyote kwa umma bila udhibiti
  au kizuizi kutoka kwa serikali. Pia huitwa uhuru wa
  kujieleza.
     Freedom of Opinion
       b. The right to express any opinion in public
       without censorship or restraint by the
       government. Also called free speech.
27. Unyanyasaji (n)
  a. Kitendo cha kumkasirisha au kumfadhaisha mtu kwa
  kumshinikiza au kwa kumsema au kumfanyia mabaya.
     Harassment
       b. The act of annoying or worrying somebody by
       putting pressure on them or saying or doing
       unpleasant things to them.
28. Wizi wa utambulisho (n)
  a. Wizi wa utambulisho hufanyika mtu anapoiba taarifa
  zako za kibinafsi kwa madhumuni ya kufanya ulaghai.
  Mwizi wa utambulisho anaweza kutumia taarifa zako
  kuomba mkopo, kutuma ripoti za kodi au kupata
  huduma za matibabu. Vitendo hivi vinaweza kuharibu
  hadhi yako ya kupata mikopo na kukugharimu wakati
  na pesa kurejesha jina lako zuri.
     Identity Theft
       b. Identity (ID) theft happens when someone
       steals your personal information to commit fraud.
       The identity thief may use your information to
       apply for credit, file taxes, or get medical services.
       These acts can damage your credit status, and
       cost you time and money to restore your good
       name.
29. Uchochezi (n)
  a. Kitendo cha kumhimiza mtu afanye jambo la vurugu,
  lililo kinyume cha sheria au baya.
     Incitement
       b. The act of encouraging somebody to do
       something violent, illegal or unpleasant.
30. Milki Dhihini (n)
  a. Wazo, muundo au kitu kama hicho ambacho mtu
  amekiunda na ambacho sheria inazuia watu wengine
  kukinakili.
     Intellectual Property
        b. An idea, a design, etc. that somebody has
        created and that the law prevents other people
        from copying.
31. Taarifa harabu (n)
  a. Habari ambayo ina msingi wa ukweli, inayotumiwa
  kudhuru mtu, shirika au nchi.
     Malinformation
        b. Information that is based on reality, used to
        inflict harm on a person, organization or country.
32. Taarifa Potofu (n) (Kutoa taarifa potofu (k)
  a. Habari zisizo sahihi juu ya jambo fulani; kitendo cha
  kutoa habari hizo zisizo sahihi.
     Misinformation
        b. The act of giving wrong information about
        something; the wrong information that is given.
33. Usawa wa Mtandao (n)
  a. Kanuni ya kuwa watoa huduma za mtandao
  wanapaswa kuruhusu ufikiaji wa tovuti na programu
  zote bila kujaribu kuzuia au kukuza tovuti au bidhaa
  fulani.
     Net Neutrality
        b. The principle that internet service providers
        should allow access to all websites and programs
        without trying to block or promote particular sites
        or products.
34. Mtandao (n)
  a. Kikundi cha watu, kampuni, n.k. kinachohusiana kwa
  karibu na ambacho hubadilishana habari na mambo
  mengine.
     Network
        b. A closely connected group of people,
        companies, etc. that exchange information, etc.
35. Usawa Mtandaoni (n)
  a. Kanuni ya kuhakikisha kwamba kila mtu anaweza
  kupata intaneti bora bila kuzingatia utambulisho wake
  wala mahali alipo.
     Network Equality
       b. A situation in which everyone has reasonable
       access to quality internet without respect to
       whom and where they are.
36. Ufikivu Huria (n/kv)
  a. Ukweli wa jambo kupatikana kwa mtu yeyote
  ambaye anautaka.
     Open access
       b. The fact of something being available to anyone
       who wants it.
37. Programu Huria (n/kv)
  a. Hutumika kueleza programu ambayo misimbo
  chanzo yake inapatikana kwa mtu yeyote bila malipo.
     Open Source
       b. Used to describe software for which the original
       source code is made available to anyone for free.
38. Ubashiri/Bashara (n)
  a. Taarifa inayosema kile unachofikiri kitatokea; kitendo
  cha kutoa taarifa hiyo.
     Prediction
       b. A statement that says what you think will
       happen; the act of making such a statement.
39. Kanuni
  a. Sheria rasmi iliyotolewa na serikali au mamlaka
  mengine.
     Regulation
       b. An official rule made by a government or some
       other authority.
40. Ugono Kisasi (n)
  a. Picha au video za mtu zinazoonyesha uchi au za
  kingono zilizochapishwa kwenye wavuti, mara nyingi
  huchapishwa na mtu aliyekuwa na uhusiano wa ngono
  naye hapo zamani, bila idhini ya mhusika na ili kumtesa
  au kumwaibisha.
     Revenge Pornography
       b. Revealing or sexually explicit images or videos
       of a person posted on the internet, typically by a
       former sexual partner, without the consent of the
       subject and in order to cause them distress or
       embarrassment.
41. Mitandao ya Kijamii (n)
  a. Tovuti na programu zinazotumiwa kwa mawasiliano
  na maingiliano ya kijamii.
     Social Media
       b. Websites and software programs used for social
       networking.
42. Udukizi (n)
  a. Ufuatiliaji wa tabia, shughuli au habari kwa kusudi la
  kukusanya taarifa, kushawishi, kusimamia au kuelekeza.
  Hii inaweza kujumuisha uchunguzi kutoka mbali
  kupitia vifaa vya kielektroniki, kama vile kamera za
  CCTV au kunyaka taarifa inayosambazwa kielektroniki,
  kama vile data inayopita mtandaoni. Inaweza pia
  kujumuisha njia rahisi za kiufundi, kama vile wanadamu
  kukusanya taarifa za kijasusi na kuiba barua za posta.
     Surveillance
       b. Monitoring of behaviour, activities, or
       information for the purpose of information
       gathering, influencing, managing or directing. This
       can include observation from a distance by means
       of electronic equipment, such as closed-circuit
       television (CCTV), or interception of electronically
       transmitted information, such as Internet traffic.
    It can also include simple technical methods, such as
    human intelligence gathering and postal
    interception.
43. Ukeraji Mtandaoni (n)
  a. Kuandika ujumbe wa uongo au wa kuchukiza kwenye
  mtandao ili kuwakasirisha wengine.
    Trolling
       b. To write false or offensive messages on the
       internet in order to make other people angry.
44. Wavuti
  a. Mtandao wa kompyuta wa mwawasiliano yenye
  taarifa mbali mbali za kimataifa.
     Internet
       b. The global system of interconnected computer
       networks that uses the Internet protocol suite to
       communicate between networks and devices.
45. Nukuu (n) /Unukuzi (kt)
  a. Mchakato wa kubadilisha maudhui ya sauti kwenye
  matangazo ya runinga au wavuti, filamu, video, CD-
  ROM, DVD, tukio linalotangazwa moja kwa moja au kazi
  zingine zilizotayarishwa kuwa maandishi na kuonyesha
  maandishi hayo kwenye skrini, kiwambo au mfumo
  mwingine wa onyesho.
     Captions
       b. The process of converting the audio content of
       a television broadcast, webcast, film, video, CD-
       ROM, DVD, live event, or other productions into
       text and displaying the text on a screen, monitor,
       or other visual display system.
46. Kisoma kiwambo (n)
  a. Kisoma kiwambo ni aina ya teknolojia saidizi ambayo
  hutoa maandishi na picha kama matamshi au breli.
  Visoma kiwambo ni muhimu sana kwa watu wenye
  ulemavu wa kutoona na huwasaidia watu wenye
  matatizo ya kuona, wasiojua kusoma na kuandika
  au wenye ulemavu wa kujifunza.
    Screen Reader
       b. A screen reader is a form of assistive technology
       (AT) that renders text and image content as
       speech or braille output. Screen readers are
       essential to people who are blind, and are useful
       to people who are visually impaired, illiterate, or
       have a learningdisability.
47. Mnemba (kv)
  a. Kuwa au kuigwa kwenye kompyuta au mtandao wa
  kompyuta, -a kutokea au kuishi mtandaoni kimsingi.
    Virtual
       b. Being on or simulated on a computer or
       computer network, occurring or existing primarily
       online.
48. Usimbaji Fiche (n)
  a. Mchakato wa kuvuruga au kufumba data ili iweze
  kusomwa tu na mtu aliye na njia ya kuirudisha katika
  hali yake ya asili.
    Encryption
       b. Encryption is the process of scrambling or
       enciphering data so it can be read only by
       someone with the means to return it to its original
       state.
49. Kikuza Kiwambo (n)
  a. Kikuza kiwambo ni programu inayoingiliana na picha
  inayotolewa na kompyuta na kuonyesha maudhui
  yaliyoongezwa ukubwa kwenye kiwambo. Kwa
  kupanua sehemu ya kiwambo (au kiwambo chote),
  watu wenye matatizo ya kuona wanaweza kuona
  maneno na picha vizuri zaidi.
    Screen Magnification software
       b. A screen magnifier is software that interfaces
       with a computer's graphical output to present
       enlarged screen content. By enlarging part (or all)
       of a screen, people with visual impairments can
       better see words and images.
50. Onyesho la Breli (n)
  a. Maonyesho ya Breli huwezesha ufikiaji wa habari
  kwenye kiwambo cha kompyuta kwa kuinua na
  kushusha mipangilio tofauti ya pini kwenye nukta
  nundu za breli kielektroniki.
     Braille Display
       b. Braille displays provide access to information
       on a computer screen for visually impaired
       people by electronically raising and lowering
       different combinations of pins in braille cells.
51. Vifaa Mbadala vya Kuingiza Data (n)
  a. Vifaa mbadala vya kuingiza data ni maunzi au
  programu zinazowawezesha watumiaji walio na aina
  mbalimbali za ulemavu kutumia kompyuta kwa njia
  tofauti. Vifaa mbadala vya kuingiza data humwezesha
  mtu mwenye ulemavu kutumia kompyuta kwa njia
  yoyote inayomfaa zaidi, kama vile kwa kutumia miguu,
  kichwa, jicho, mdomo, pumzi, kidole gumba au kidole
  kimoja.
     Alternate Input Devices
       b. Alternative input devices are hardware or
       software solutions that allow users with a variety
       of disabilities or impairments to access a
       computer in a different way. Alternative input
       devices allow the user to access a computer in
       whatever way works best for them such as using
       his/her feet, head, eye, mouth, breath, thumb, or a
       single finger.
52. Nyongezo kicharazio (n)
  a. Programu au vifaa vinavyoongezwa kwenye
  vicharazio vya kompyuta ili kuvifanya viweze kutumika
  na watu wenye ulemavu.
     Keyboard enhancements
       b. Software or hardware that is added to
       computer keyboards in order to make them
       accessible to persons with disabilities.